Matumizi ya Fantasia katika Usanaji wa Filamu za Kiswahili Nchini Tanzania

Abstract

Makala hii inahusu matumizi ya fantasia katika usanaji wa filamu za Kiswahili nchini Tanzania. Fantasia ni miongoni mwa vipengele vinavyohusishwa na uhalisiajabu ambavyo hutumiwa na watunzi kusana kazi zao. Utafiti uliozaa makala hii ulitumia mbinu za kitaamuli. Data zilikusanywa kwa kutumia mbinu za uchambuzi matini na mahojiano. Filamu teule zilipatikana kwa kutumia mbinu ya usampulishaji lengwa. Uchambuzi wa data za makala umefanyika kwa kutumia Nadharia ya Fantasia. Filamu za Kiswahili za Kitanzania za Jamila na Pete ya Ajabu na Nsyuka zimetumika kama sampuli ya kubainisha mdhihiriko wa fantasia. Maeneo ambayo ufantasia umejitokeza katika filamu teule yamebainishwa. Maeneo hayo yamehusisha matukio ya kihadithi ya filamu pamoja na uwasilishaji wa ujumbe kupitia uigizaji. Aidha, ilibainika kuwa fantasia hutumika katika kuunda filamu kwa malengo ya ujengaji wa taharuki, ubunifu, na usisimuaji wa hisia ya mtazamaji. Vilevile, ilibainika kuwa matumizi ya fantasia katika filamu teule yana tija na madhara kwa usanaji na uwasilishaji wa filamu za Kiswahili kwa hadhira. Kufuatia matokeo haya, inapendekezwa watayarishaji wa filamu kuzingatia uwiano wa matumizi ya fantasia katika filamu ili kuepusha madhara yaliyoelezwa katika makala hii.

Download

PDF