Mdhihiriko wa Anthroposenia katika Riwaya za Bustani ya Edeni na Vipuli vya Figo: Misukumo ya Tamaa na Ulofa

Abstract

Makala hii inahusu uchanganuzi wa namna anthroposenia inavyodhihirika katika riwaya mbili za Emmanuel Mbogo, Bustani ya Edeni na Vipuli vya Figo, kwa kujikita katika misukumo ya tamaa na ulofa. Kusudi la makala hii ni kujadili mchango wa binadamu katika kukuza anthroposenia kupitia tamaa na ulofa. Mtindo wa uchambuzi wa maandishi ya fasihi ulitumika katika ukusanyaji wa data. Ukusanyaji na uchanganuzi wa data uliongozwa na Nadharia ya Uhakikimazingira iliyoasisiwa na Glotfelty & Fromm (1996). Nguzo zilizoongoza uchanganuzi huu ni binadamu dhidi ya maumbile, uwezo, na maendeleo endelevu. Kisha, data ilidondolewa kutoka kwenye riwaya mbili teule na kuchanganuliwa kupitia njia ya upekuzi-changanuzi wa maudhui kwa kuongozwa na nguzo tatu za Nadharia ya Uhakikimazingira. Hatimaye, ilidhihirika kuwa athari za viwanda vya kemikali katika uharibifu wa mazingira pamoja na tamaa na ulofa ni mazao ya shughuli za kila siku za binadamu katika kupalilia anthroposenia ulimwenguni. Makala hii imeonesha jinsi mtunzi, Mbogo, anavyotumia fasihi kuonya kuhusu madhara ya binadamu kwa mazingira, huku akihimiza mabadiliko ya mielekeo, mawazo na matendo kwa lengo la kuyahifadhi mazingira. Matokeo ya makala hii yanatoa mchango muhimu katika masuala ya kimazingira na maadili ya kisasa pamoja na kudhihirisha nafasi ya riwaya ya Kiswahili katika kuelezea na kupinga changamoto za anthroposenia.

Download

PDF

Keywords

Anthroposenia
,
shughuli
,
tamaa
,
ulofa