Abstract
Makala hii inajadili nafasi ya fasihi andishi katika ukuzaji wa stadi za mawasiliano katika shule za sekondari teule wilayani Nyanza nchini Rwanda. Ili kutimiza lengo hili, Nadharia ya Mawasiliano ya Scudder (1980) imetumiwa. Aidha, katika ukusanyaji data, mbinu za usaili, ushuhudiaji na uchambuzi matini zilitumiwa. Wango la utafiti lilihusisha walimu wa Kiswahili na wanafunzi wanaojifunza kwenye mchepuo wa Fasihi katika Kiingereza, Kifaransa, Kiswahili na Kinyarwanda (LFK). Mbinu ya usampulishaji lengwa ilitumiwa ili kupata sampuli ya walimu 9 na wanafunzi 93. Makala inabainisha kwamba fasihi andishi ina nafasi katika ukuzaji wa uwezo wa mawasiliano, stadi za lugha, ujasiri na utambuzi wa hisia. Pia, sehemu kubwa ya walimu wa Kiswahili haijafanikiwa kutumia fasihi andishi katika kukuza stadi za mawasiliano katika Kiswahili miongoni mwa wanafunzi wao; badala yake hujikita zaidi katika kufundisha dhana za nadharia ya fasihi. Aidha, makala inabainisha kuwa walimu wa shule teule hawajumuishi kikamilifu fasihi andishi katika mbinu zao za ufundishaji, wakizingatia zaidi kanuni za fasihi na kupuuza mazoezi ya mawasiliano ya kina. Tathmini za walimu zinaangazia zaidi stadi za kusoma na kuandika, huku zikipuuzia stadi nyingine kama vile kusikiliza, kuzungumza, ujasiri na utambuzi wa hisia ambazo ni stadi muhimu katika mawasiliano.