Abstract
Makala hii inahusu upokezi wa istilahi za BAKITA katika somo la Sayansi na Teknolojia kwa watumiaji. Lengo ni kufafanua sababu za kupokelewa na kutopokelewa kwa istilahi za BAKITA na athari zake katika somo la sayansi na teknolojia darasa la VI. Data zilipatikana kwa njia ya uchambuzi matini na usaili na kuchambuliwa kwa Nadharia ya Istilahi za Kisayansi ya Kiingi (1989). Makala imeonesha matokeo ya aina tatu ambayo ni: kupokelewa kwa baadhi ya istilahi kwa walengwa wake, kutopokelewa kwa baadhi ya istilahi kwa walengwa wake, na athari zake. Kupokelewa kumechagizwa na sababu tatu. Nazo ni uzoefu wa istilahi husika kwa watumiaji wake, uwezo wa istilahi kubeba dhana husika, pamoja na mbinu iliyotumika kuunda istilahi husika. Kutopokelewa kwa istilahi kumechagizwa na sababu nne. Nazo ni dhana moja kurejelewa na istilahi tofauti, kasi ndogo ya uchapaji na usambazaji wa istilahi, tofauti ya tahajia ya istilahi za sayansi na teknolojia pamoja na ugeni wa istilahi husika kwa watumiaji. Kutopokelewa kwa istilahi husababisha kuwapo kwa istilahi zisizotumiwa na kutumika kwa istilahi zisizosanifishwa. Kutokana na matokeo hayo, makala hii inapendekeza kuzingatiwa kwa mikakati ya kupokelewa kwa istilahi kwa watumiaji wake. Mikakati hiyo ni kuhakikisha istilahi zilizoundwa zinawafikia walengwa wake na kufanya tathmini ya istilahi zilizoundwa.