Mawanda na Mazingira ya Utokeaji wa Kirai Kihusishi katika Sentensi za Kiswahili

Abstract

Utambuzi na ubainishaji wa kirai kihusishi katika sentensi za Kiswahili unaibua mgogoro wa kimtazamo, miongoni mwa wanasarufi wa lugha hii, kuhusu mawanda na mazingira ya utokeaji wa kirai hicho. Mawanda hayo ni Kngo+H, Kngo+H+Kngo na H+Kngo. Kujiegemeza katika mawanda haya kumechagiza dosari kadhaa katika utambuzi wa kirai hiki na aina zingine za virai. Kwa hiyo, makala hii inalenga kudhihirisha mawanda na mazingira ya utokeaji wa kirai kihusishi katika sentensi za Kiswahili. Utafiti unaoripotiwa katika makala hii ulifanyika maktabani na uwandani. Mbinu zilizotumika kukusanya na kuchambua data ni usomaji matini kutoka Riwaya ya Nagona ya Kezilahabi (2011), upimaji wa usahihi wa kisarufi, na usaili. Mkabala wa Kileksika ulioasisiwa na Lewis (1993) ulitumika katika kufasiri na kuchanganua data za utafiti uliozaa makala hii. Matokeo yanaonesha kuwa mawanda ya kirai kihusishi huanzia kwenye kihusishi na hukomea katika kirai nomino cha baada yake. Vilevile, kirai hiki hutokea baada ya nomino, kitenzi, kibainishi, kivumishi, kiwakilishi, kuhusishi au kiunganishi katika sentensi za Kiswahili. Msimamo wa makala hii ni katika mawanda ya H+Kngo kwa sababu mawanda haya ndiyo yanayoakisi mawanda ya virai vingine vya Kiswahili. Kwa hiyo, usahihi wa utambuzi na ubainishaji wa kirai hiki unatoa uwezekano wa uainishaji wa viambajengo vingine vya sentensi kwa usahihi.

Download

PDF

Keywords

Kirai kihusishi
,
sentensi
,
mazingira
,
mawanda
,
mkabala wa kileksika