Abstract
Kiswahili ni miongoni mwa lugha kubwa zenye wazungumzaji wengi barani Afrika na hata nje ya bara la Afrika (Kishe, 2017). Nchini Tanzania, serikali pamoja na vyombo mbalimbali vya kukuza na kueneza Kiswahili kama vile BAKITA, BAKIZA, vyuo vikuu na vyama mbalimbali vya Kiswahili vimekuwa vikiendelea kufanya jitihada mbalimbali katika kukikuza, kukiendeleza na kukieneza Kiswahili nchini na hata nje ya nchi. Pamoja na jitihada hizo, bado kumekuwa na changamoto za kukifanya Kiswahili kiwe bidhaa katika soko la ndani na nje ya Afrika (Cherono & Ogechi, 2018). Makala hii inakusudia kuzielezea changamoto hizo, hususani zinazowakabili wahitimu wa vyuo vikuu wa shahada za sanaa katika Kiswahili. Utafiti uliozaa makala hii uliongozwa na Nadharia ya Ubidhaishaji. Mbinu ya mahojiano ndiyo iliyotumika katika kukusanya data. Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa wahitimu wa Kiswahili wanakabiliana na changamoto zitokanazo na ukosefu wa maarifa ya TEHAMA, ukosefu wa elimu ya kijasiriamali, ukosefu wa mtaji, ushindani, na hofu na kukata tamaa. Kutokana na changamoto hizo, makala inapendekeza kuwa serikali, kupitia sekta ya elimu, ihimize watunga sera wa elimu kuboresha mitaala ya masomo ya lugha ya Kiswahili kuanzia shule za msingi mpaka vyuo vikuu.