Usawiri wa Ukizinda kwa Mawanda ya Mtu katika Riwaya ya Kiswahili: Mifano kutoka Rosa Mistika na Harusi

Abstract

Makala hii inajadili ukizinda wa Waswahili katika riwaya za Rosa Mistika (1971) na Harusi (1984). Kwa ujumla, dhana ya ukizinda hujadiliwa katika mielekeo mikuu mitatu: vitu vya asili, sanaa, na mtu. Kwa muktadha wa makala hii, tunaitambulisha mielekeo hii kama mawanda. Lengo la makala hii ni kujadili vipengele vinavyozingatiwa na jamii za Waswahili katika kuuthamini ukizinda kwa mawanda ya mtu. Unapotazamwa katika mawanda haya, ukizinda hurejelea hali anayokuwa nayo mwanamke ambaye hajawahi kukutana kimwili na mwanamume. Utafiti uliozaa makala hii uliongozwa na Nadharia ya Sosholojia ya Fasihi. Data zilikusanywa kwa kutumia njia ya uchambuzi wa matini na usaili. Makala inabainisha kwamba ukizinda katika mawanda ya mtu katika jamii za Waswahili huangaliwa kupitia vipengele vinne. Navyo ni: kutambua umuhimu wa kizinda, kulinda kizinda, kutafuta kizinda, na kupima kizinda. Kwa kuwa ukizinda katika jamii za Waswahili huchukuliwa kama kitu chenye thamani, hususani katika kipengele cha maadili, makala inapendekeza kuwa tafiti zaidi zifanyike kuhusiana na masuala ya ukizinda wa Waswahili kupitia tanzu zingine za fasihi ya Kiswahili. Aidha, utafiti linganishi unaweza ukafanyika kutoka jamii za Waswahili na nyingine ili kuona tofauti ya chukulizi zilizopo katika jamii hizo kuhusiana na masuala ya ukizinda katika mawanda ya mtu.

Download

PDF

Keywords

ukizinda
,
mawanda
,
mtu
,
Waswahili