Abstract
Makala hii inachunguza kwa nini baadhi ya nomino za Kiswahili zina viambishi-awali vyenye irabu ndefu ilhali viambishi-awali hivyohivyo vikisikika kuwa na irabu fupi kwenye nomino zingine. Irabu ndefu za viambishi-awali si jambo geni kwenye nomino za Kiswahili. Zinaweza kusababishwa na milolongo ya konsonanti au kuungana kwa irabu. Hata hivyo, si kila irabu ndefu kwenye viambishi-awali vya nomino hutokana na michakato hiyo. Utafiti ulifanywa ili kujua sababu zingine za kutokea irabu ndefu kwenye viambishi-awali vya baadhi ya nomino za Kiswahili. Data zilikusanywa kutoka maandikoni na uwandani, zikiwa nomino zenye viambishi-awali vilivyo na irabu. Nomino hizo zilitamkwa na wasemaji wa Kiswahili wa Zanzibar. Matamshi yao yalichakatwa kwa programu ya kompyuta ili kubainisha nyakaa za irabu zinazotokea kwenye viambishi-awali. Uchanganuzi wa data uliongozwa na dhana ya urefu, urefushaji, na ufupishaji. Matokeo ya uchanganuzi yanaonyesha kuwapo kundi dogo la nomino za Kiswahili zenye viambishi-awali vyenye irabu ndefu. Inadhaniwa kuwa irabu hizo ndefu zilisababishwa na ruwaza za toni zilizokuwapo katika Mame-Bantu. Ingawa Kiswahili kimeshapoteza ruwaza za toni kilizozirithi kutoka Mame-Bantu, inadhaniwa kuwa nacho kilikuwa kikirefusha irabu za viambishi-awali vya baadhi ya nomino ili zitangamane na ruwaza za toni kwenye maumbo ya baadhi ya nomino za lugha hiyo ya kale. Kuwapo kwa nomino hizi chache zenye viambishi-awali vyenye irabu ndefu ni ushahidi mmojawapo uliobaki wa kuwapo kwa ruwaza za toni katika Kiswahili baada ya kutokea mabadiliko ya kihistoria katika lugha hii.