Abstract
Makala hii inajadili mbinu mbalimbali za usimulizi zinazotumika katika vibonzo jongevu na sababu za kutumika kwake. Makala inabainisha kuwa watunzi hutumia mbinu zifuatazo za usimulizi: usimulizi wa moja kwa moja, usimulizi wa kuhamahama, usomaji wa kitabu, usimulizi wa ndotoni, pamoja na mbinu za kisasa kama usimulizi wa kiteknolojia na matumizi ya ujumbe mfupi. Aina hizi za usimulizi zinasaidia kuunganisha matukio, kusisitiza maudhui, ujenzi wa taharuki, kuhamasisha watoto kupenda kusoma, na kuendeleza utamaduni. Kupitia mifano mbalimbali kutoka katika vibonzo jongevu, makala imebainisha kuwa matumizi ya usimulizi katika vibonzo jongevu hutumika kufafanua hisia na matukio yasiyoelezwa na wahusika, kuunganisha na kusimamia mtiririko wa hadithi, kuelekeza tafsiri ya matukio kwa watazamaji, kutoa mtazamo mpana kwa kueleza hali na mawazo ya wahusika wote, pamoja na kuunda mtindo na utambulisho wa kipekee wa kazi husika. Data zilizozaa makala hii zimepatikana maktabani, ambapo mwandishi alitazama kazi mbalimbali za vibonzo jongevu na kuzifanyia uchambuzi kulingana na mahitaji yake. Nadharia ya Usimulizi wa Fasihi Simulizi imemwongoza mwandishi katika kukusanya na kuchambua data zake. Makala inahimiza ubunifu zaidi katika matumizi ya mbinu hizi kwa maendeleo ya watoto, hasa katika zama hizi za kidijiti ambapo teknolojia ni nyenzo muhimu ya uwasilishaji wa fasihi ya watoto.