Abstract
Makala hii inafafanua thamani ya kimawasiliano inayopatikana katika ufyosi wa kimaandishi. Hoja kuu ya makala ni kudhihirisha kuwa, licha ya umbo la nje la ufyosi kubeba uhasi na, hivyo, kupingwa na maadili ya jamii nyingi, kipengele hiki kina thamani kubwa katika jamii. Hii ndiyo sababu inayokifanya kiendelee kutamalaki katika mawasiliano ya watu. Matukio ya ufyosi yaliyotumika ni yale yanayosawiriwa kupitia jumbe za WhatsApp. Data zilikusanywa kupitia jumbe za WhatsApp zilizoingia katika simu za waandishi (kupitia akaunti binafsi pamoja na makundi mbalimbali ambayo waandishi wa makala wamo kama wajumbe). Swali muhimu lililoongoza utafiti uliozaa makala hii ni: Je, ufyosi unaopatikana katika jumbe za WhatsApp una thamani ipi ya kimawasiliano? Utafiti na mjadala vimefanywa kwa kutumia misingi ya nadharia ya upokezi. Matokeo yanaonesha kuwa ufyosi hubeba thamani mbalimbali, zikiwamo kudhihirisha ujumi, kudhihirisha ukaribu/uhusiano wa wahusika wanaowasiliana, kudhihirisha tabia ya mtandaoni, kulainisha maisha, pamoja na kufumba mambo.