Ninaelewa, kwa hiyo, Ninaamua na Kuchagua: Demokrasia, Kiswahili na Maendeleo ya Wananchi wa Tanzania

Demokrasia, Kiswahili na Maendeleo ya Wananchi wa Tanzania

Abstract

Makala inachambua dhana ya demokrasia, lugha ya Kiswahili, na maendeleo ya wananchi. Inaangalia demokrasia inavyoweza kujengwa na lugha; na kuwafanya wananchi kujitambua na kuchukua hatua kujiletea maendeleo. Makala inajadili kuwa, mosi, jitihada za kuwafanya wananchi waweze kushiriki katika mchakato wa kidemokrasia lazima zilenge kuwafanya wananchi hao kuelewa kile wanachokitaka wao wenyewe. Pili, ili kufanikisha ukombozi wowote, ni lazima wananchi wawe na uelewa wa kifikra na kujitambua. Kuelewa na kujitambua hufanikishwa kupitia mawasiliano yanayotokana na lugha inayochipuka katika mazingira na utamaduni wa wananchi husika. Bila kuelewa hakuna kujitambua, na itakuwa vigumu kushiriki katika demokrasia. Bila kuelewa hakuna maendeleo. Bila mtu kuweza kuyaelewa mazingira yake na kuyamudu, hakuwezi kukawa na ukombozi wa kweli. Kieneo, makala hii imekitwa nchini Tanzania kama kiwakilishi cha maeneo mengine yanayotumia lugha ya Kiswahili barani Afrika.   Makala inatumia Nadharia ya Ubaadaukoloni katika kujadili dhana ya demokrasia kwa kutumia mkabala wa lugha ya Kiafrika. Tutaonesha kuwa lugha ya Kiswahili inaweza kuwapatia wananchi uelewa na kuwasaidia kushiriki kikamilifu katika kujenga na kuimarisha demokrasia. Tunalenga kuonesha kuwa, kupitia lugha inayoeleweka, wananchi wataimarika kidemokrasia na watashiriki katika kujiletea maendeleo.

Download

PDF