Mchango wa Fonolojia katika Kuuelewa Ushairi Andishi wa Kiswahili

Abstract

Wataalamu mbalimbali wanabainisha kuwa kueleweka kwa ushairi kunategemea sana kuielewa fani kwa kuwa ndio nyenzo iwasilishayo maudhui. Kwa mintarafu hii, hatuna budi kuvielewa vipengele mbalimbali vya kifani vilivyotumika katika mashairi husika kama vile tamathali za semi, picha na ishara, muundo, mtindo na wahusika (Wamitila, 2004 na Mulokozi, 2017). Hata hivyo, wataalamu wengine wanabainisha wazi kuwa kazi yoyote ya fasihi, ukiwamo ushairi, hutumia lugha kuwasilisha maudhui hayo. Hivyo, ili kuyaelewa maudhui yanayowasilishwa na mashairi, uchambuzi wa lugha iliyotumika ni suala muhimu sana (Njogu na Chimerah, 2008). Aidha, ifahamike kuwa kueleweka kwa mashairi kunategemea sana kueleweka kwa vipengele mbalimbali vya kisarufi (kama vile vya kifonolojia, kimofolojia, kisintaksia na kisemantiki) vilivyotumika katika shairi husika. Kutokana na hilo, makala hii inafafanua mchango wa fonolojia katika kueleweka kwa ushairi. Ili kufanya hivyo, makala hii imechambua vipengele mbalimbali vya kifonolojia vilivyomo katika vitabu viwili, Mashairi ya Saadani (1972) na Malenga wa Bara (1976). Utafiti uliozalisha makala hii ulikuwa wa maktabani, na uwandani. Aidha, data zilikusanywa kwa kutumia mbinu ya uchambuzi matini na ushuhudiaji. Uchambuzi na uwasilishaji wa data ulizingatia Nadharia ya Umuundo.Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa fonolojia ina mchango mkubwa katika kuuelewa ushairi kupitia vipengele vya mpangilio wa fonimu na uradidi wake katika ushairi, uradidi wa silabi, wizani, mkazo na kiimbo.

Download

PDF