Abstract
Utenzi wa Mwana Kupona umevuta nadhari kubwa kwa wasomaji na wahakiki wengi wa kazi za fasihi. Tafiti nyingi zimefanywa kuhusu utenzi huo kwa kukitwa katika mitazamo mikuu mitatu. Mtazamo wa kwanza, unaouona utenzi huo kuwa unamdhalilisha mwanamke; wa pili unautazama kuwa ni utenzi unaosawiri maisha halisi ya mwanamke wa pwani. Mtazamo wa tatu unautazama kama ni kielelezo cha kumdhalilisha mwanamume. Pamoja na tafiti hizo kuweka misingi katika kuuelewa utenzi huo, mtazamo wa tatu unatoa chachu kwa mtafiti kuchunguza kwa kina ni kwa namna gani utenzi huo unamtweza mwanamume. Hii inatokana na kwanza; msukumo unaotolewa na Mbele (1985) ambaye kupitia utenzi huo, anabainisha kuwa kazi ya fasihi ina mawanda mapana ya kiuhakiki na, hivyo, kuwaasa wasomaji wasiwe na mtazamo funge pindi wanapohakiki kazi hizo. Pili, mjadala anaouzua Mulokozi (1999) kwa kuuliza kama utenzi huo unamdhalilisha mwanamke au mwanamume. Tatu, mijadala iliyofanywa kuhusiana na mtazamo wa namna utenzi huo unavyomdhalilisha mwanaume kwa mfano ule wa Mbele (1985) umegusia suala hilo kwa jumla pasipo kufafanua kwa kina vipengele vinavyomdhalilisha mwanamume katika utenzi huo. Uandishi wa makala umezingatia mkabala wa kitaamuli. Data za msingi zilikusanywa maktabani kutoka katika kitabu cha Tenzi Tatu za Kale na uwandani. Kwa kutumia misingi ya nadharia ya Mwitiko wa Msomaji, makala imethibitisha hoja ya msingi kuwa, Utenzi wa Mwana Kupona ni kilingo cha kumtweza mwanamume. Hii inatokana na namna mwandishi anavyomjenga mwanamke kwa kumfanya kuwa kiongozi, msaada na nguzo msingi katika maamuzi ayafanyayo mwanamume.