Dhima za Kialami Pragmatiki ‘mh’ katika Mazungumzo ya Kiswahili

Abstract

Makala hii inachunguza dhima za kialami pragmatiki mh katika mazungumzo ya Kiswahili. Data ya makala hii imekusanywa kutoka katika mazungumzo yasiyo rasmi ya Kiswahili yanayofanywa katika maeneo yasiyo rasmi. Maeneo hayo ni kama kwenye vijiwe vya kahawa na vijiwe vya mamantilie. Uchambuzi wa data za makala hii umeongozwa na Nadharia ya Umuktadhaishaji ya Gumperz (1982). Matokeo ya utafiti huu yanaonesha kwamba kialami pragmatiki mh huchanuza maana tofautitofauti kulingana na muktadha kinamotumika. Kwa hiyo, kialami pragmatiki hicho huwa na dhima mbalimbali za kipragmatiki. Baadhi ya dhima hizo ni kama vile kuashiria kuitika, kumtaka mzungumzaji arudie kauli au swali, kumjulisha mshiriki mwingine wa mazungumzo apokee au achukue kitu, kudokeza kwamba mzungumzaji anaanzisha mazungumzo, kumruhusu mzungumzaji mwingine aendelee kuzungumza, kutumika kama jibu la swali na kuonesha hisia mbalimbali kama vile dharau na mshangao. Kwa ujumla, makala hii inaadokeza kwamba vialami pragmatiki vina dhima mbalimbali katika lugha ya Kiswahili. Hivyo, tafiti zaidi zifanyike ili kubaini dhima za vialami pragmatiki vingine katika lugha hii. Aidha, kialami pragmatiki mh kinaweza kuchunguzwa zaidi kwa kuhusisha na taaluma za fonolojia na fonetiki ili kubaini ruwaza zake na athari zake kwenye maana za kialami hicho.

Download

PDF