Ufafanuzi Linganishi wa Kimofolojia katika Mizizi ya Vitenzi vya Kiswahili vyenye Asili ya Kiarabu na vile vya Kiswahili Asilia

Abstract

Makala hii inahusu ufafanuzi linganishi wa kimofolojia katika mizizi ya vitenzi vya Kiswahili vyenye asili ya Kiarabu na vile vya Kiswahili asilia. Lengo la ulinganishi huu ni kuweka wazi kufanana na kutofautiana kwa mizizi hiyo ili kuonesha mipaka iliyopo katika uchanganuzi wa vitenzi hivyo. Ulinganishaji huo umefanyika kwa kutumia data ya vitenzi iliyopatikana katika Kamusi Kuu ya Kiswahili ya BAKITA (2017). Pia, mifano na ufafanuzi uliotolewa na wataalamu mbalimbali kuhusu mizizi ya maneno ya Kiswahili imesaidia kuonesha ukweli kuhusu mizizi ya vitenzi vya Kiswahili asilia. Data hiyo imeshughulikiwa kwa kuzingatia kiunzi cha Nadharia ya Mofolojia Leksika, ambapo mihimili miwili ya nadharia hiyo imehusishwa. Mihimili iliyohusishwa ni kanuni ya kufuta mabano na kanuni ya mzunguko kamili. Kwa hiyo, ufanano na utofauti wa vitenzi hivyo umedhihirika. Katika mazingira kadhaa, mizizi ya vitenzi vya Kiswahili vyenye asili ya Kiarabu vimefanana na vya Kiswahili asilia kutokana na utegemezi wa mizizi yake na katika baadhi ya miundo ya mizizi. Pia, vitenzi vya Kiswahili vyenye asili ya Kiarabu vimetofautiana na vile vya Kiswahili asilia kutokana na vitenzi hivyo kuwa na mizizi huru michache na baadhi ya miundo ya mizizi hiyo kutofautiana.

Download

PDF