Fokasi: Misingi ya Uainishaji, Mbinu za Ung’amuzi na Mikakati ya Usimbaji katika Sentensi za Kiswahili

Abstract

Fokasi ni mojawapo ya kiambajengo cha kipragmatiki katika lugha ya Kiswahili. Uainishaji wa fokasi, mbinu za ung’amuzi wa fokasi na mikakati na usimbaji wa fokasi hutofautiana kutoka lugha moja hadi nyingine. Hata hivyo, katika lugha ya Kiswahili, masuala hayo hayapo bayana. Kwa hiyo, makala hii imeshughulikia misingi ya uainishaji wa fokasi, mbinu za ung’amuzi wa fokasi na mikakati ya usimbaji wa fokasi katika lugha ya Kiswahili. Data ya makala hii imekusanywa kwa kutumia mbinu ya usimulizi wa picha. Aidha, tumetumia mkabala wa kitaamuli katika uchambuzi wa data ya makala hii huku tukiongozwa na Nadharia ya Semantiki Vibadala iliyoasisiwa na Rooth (2016). Matokeo yameonesha kuwa kuna misingi minne ya uainishaji wa fokasi katika sentensi za Kiswahili. Misingi hiyo ni mazingira ya utokeaji, muundo, semantiki na lengo la mawasiliano. Aina za fokasi zilizobainika  hung’amuliwa kwa kutumia mbinu ya maswali na majibu, usahihishaji wa taarifa au vibainishi vya fokasi. Vilevile, imebainika kuwa fokasi husimbwa katika sentensi za Kiswahili kwa kutumia mkakati wa ukasimishaji, utenguaji kushoto, unyambuaji punguzi wa vishiriki vya kitenzi, uhamishaji wa viambajengo au uwekaji wa mkazo katika tungo. Pamoja na hayo, tunapendekeza utafiti mwingine kufanyika ili kuchunguza usimbaji wa fokasi katika vipera vya fasihi simulizi kama vile nahau na hadithi.

Download

PDF