Utumizi wa Mbinu za Fasihi Simulizi katika Nyimbo za Injili: Mfano kutoka Wimbo wa Bahati Bukuku Uitwao “Kampeni”

Abstract

Makala hii imeangalia kwa kina utumizi wa mbinu za fasihi simulizi ya Kiswahili katika nyimbo za injili kwa kutumia wimbo uitwao ‘Kampeni’ wa Bahati Bukuku uliohifadhiwa katika picha jongefu. Nadharia ya uhakiki wa kimtindo imetumika kufafanua matini katika uchambuzi wa kazi hii ya fasihi. Katika wimbo huu, mbinu mbalimbali za fasihi simulizi zimetumika kuijenga kazi hii. Kupitia picha jongefu, mhusika mkuu anatumia njia ya majigambo, chuku na kejeli ambavyo ni nduni za fasihi simulizi. Wimbo huu pia unatawaliwa na usimulizi. Usimulizi huu wa kifasihi ingawa umekusudiwa kutoa mafundisho, umechota kwa sehemu kubwa sifa anuai za fasihi simulizi na kuziingiza katika matumizi ya injili. Katika wimbo huu pia, kuna mandhari mbalimbali zilizotumika kibunilizi kama vile: mandhari ya duniani, Jehanamu na mbinguni. Fanani katika wimbo huu anaruhusu wahusika watokee kama vionwa katika picha hiyo jongefu lakini maneno yote yasemwe na yeye msimuliaji. Wimbo huu unaonesha kuwa fasihi simulizi inaouwezo wa kubadili uwasilishwaji wake na kuifanya ikidhi matakwa mbalimbali ya jamii. Kupitia wimbo huu ni bayana kuwa fasihi simulizi inakubali mabadiliko na kuifanya iingie katika nyanja anuai kama katika picha jongefu za muziki wa injili.

Download

PDF