Utendaji katika Vichekesho Vinavyowasilishwa kwa Njia ya Elektroniki: Uchunguzi wa Vichekesho vya Ze Orijino Komedi

Abstract

Makala hii imelenga kujadili mbinu za kiutendaji katika vichekesho vinavyowasilishwa kielektroniki. Uchunguzi huu ulichochewa na mgongano wa mawazo kuhusu sifa ya utendaji inavyoathiriwa na mabadiliko ya uwasilishaji wa kazi za fasihi, hususani fasihi simulizi. Data za makala hii zilikusanywa kutoka katika vichekesho teule vya Ze Orijino Komedi vilivyohifadhiwa katika mtandao wa YouTube. Data hizo zilifafanuliwa na kuchambuliwa kwa kutumia mkabala wa kimaelezo huku tukiongozwa na Nadharia ya Utendaji iliyoasisiwa na Dan-Ben-Amos (1972). Nadharia hii imetuongoza kubaini mbinu mbalimbali za kiutendaji zilizotumika katika vichekesho teule vya Ze Orijino Komedi vilivyo katika mtandao wa YouTube. Matokeo yameonesha uwasilishaji wa vichekesho kwa njia ya elektroniki umesababisha fanani na hadhira kutokuonana ana kwa ana. Hata hivyo, utendaji katika kazi hizi umeendelea kuwapo. Matokeo haya yalifikiwa kutokana na kujitokeza kwa vipengele mbalimbali vya kiutendaji kama vile matumizi ya ishara, uigizaji wa sauti na matendo, matumizi ya maleba, matumizi ya muziki, ushiriki wa hadhira na matumizi ya lugha ya kisanaa. Kutokana na matokeo hayo, imehitimishwa kwamba mabadiliko ya uwasilishaji wa kazi za fasihi, hususani fasihi simulizi, si uasi bali yanadhihirisha uhai wake. Aidha, uhai huo unatokana na uwezo wa fasihi kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia bila kupoteza sifa ya utendaji.

Download

PDF