Mtazamo kuhusu Wakati katika Falsafa ya Kiafrika: Mifano kutoka Riwaya Teule za Kiswahili

Abstract

Waafrika kama zilivyo jamii nyinginezo duniani wana falsafa inayoongoza maisha yao. Katika uga wa fasihi, wataalamu mbalimbali wametafiti na kuangalia namna falsafa hiyo inavyodhihirika kupitia vipengele mbalimbali vya maisha. Hata hivyo, mtazamo kuhusu wakati kama kipengele kinachoibua Falsafa ya Waafrika, kwa kuhusisha udhihirikaji wake na vipengele vingine vya kifalsafa hakijamakinikiwa vya kutosha. Jambo hili linasababisha ufinyu wa mawanda katika kuelewa mtazamo wa falsafa ya wakati, uhusiano wake na vipengele vingine vya kifalsafa pamoja na athari zake kwa jamii ya Waafrika. Kwa kuzingatia pengo hilo la kimaarifa, makala hii imekusudiwa kubainisha mtazamo kuhusu wakati kwa Waafrika kama unavyodhihirika kupitia vipengele mbalimbali vya kifalsafa pamoja na athari zake kwa jamii. Data za makala hii zilikusanywa maktabani na uwandani. Nadharia ya Ontolojia ya Kiafrika ilitumika katika uchanganuzi na uwasilishaji wa matokeo ya utafiti. Kwa ujumla, makala inabainisha kuwa mtazamo kuhusu wakati ni kipengele muhimu sana kwa Waafrika kwani una athari kubwa kwa namna wanavyoyaendesha maisha yao. Waafrika wanaamini kuwa wakati ni kiini cha ‘kuwapo’ kwa mwanadamu kunakojibainisha kupitia vipengele mbalimbali katika maisha kama vile uzazi, maisha baada ya kifo pamoja na busara na hekima ambazo huaminika kuwapo kwa wazee walio hai pamoja na waliokufa.

Download

PDF