Ruwaza ya Vitenzi vya Kibantu katika Muktadha wa Vitenzi vya Kiswahili

Abstract

Makala hii inahusu ruwaza ya vitenzi vya Kibantu katika muktadha wa vitenzi vya Kiswahili. Lengo la makala hii ni kuonesha utokeaji wa viambishi vya ruwaza ya vitenzi vya Kibantu katika Kiswahili iwapo vinajitokeza vyote au la na matumizi ya viambishi hivyo katika Kiswahili. Hili linasaidia kuongeza zaidi maarifa katika mofolojia ya Kiswahili na kuendelea kuthibitisha Ubantu wa Kiswahili.  Lengo hilo limetimizwa kwa kutumia data ya mifano ya vitenzi vyenye viambishi mbalimbali vilivyokusanywa katika baadhi ya vitabu vya mofolojia ya Kiswahili.  Kwa hiyo, kutokana na mifano hiyo ya vitenzi vilivyochanganuliwa kwa kutumia mhimili wa kufuta mabano wa Nadharia ya Mofolojia Leksika, yafuatayo yamebainika: Kiswahili kinabeba viambishi vingi vya ruwaza ya vitenzi vya Kibantu, isipokuwa viambishi vichache ambavyo havidhihiriki kabisa katika Kiswahili. Viambishi hivyo ni kama viambishi awali tangulizi vya uwakilishi. Pamoja na hayo, kuna baadhi ya viambishi vya ruwaza hiyo vinavyotokea katika Kiswahili vikiwa na mazingira maalumu ya utokeaji wake kama kiambishi tamati tangulizi na baadhi ya viambishi tamati vya ziada. Kwa hiyo, kiambishi tamati tangulizi na baadhi ya viambishi tamati vya ziada vinaweza kuchunguzwa zaidi. Hii itasaidia kuona mazingira mbalimbali ya utokeaji wa baadhi ya viambishi hivyo katika Kiswahili.

Download

PDF