Utendeza Unavyoathiri Urefu wa Irabu katika Kiswahili Sanifu

Abstract

Makala hii inachunguza namna viambishi tamati vya utendeza, {-z-, -ez-, -iz-}, vinavyoathiri urefu wa irabu za neno pindi vinapoambatishwa kwenye mashina ya vitenzi vya Kiswahili Sanifu (KS). Data za utafiti huu zilikusanywa maktabani katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), kwa mbinu ya upitiaji nyaraka; na uwandani, huko Mji Mkongwe, Zanzibar, kupitia usaili. Data zilikuwa vidahizo vya KS vyenye uambishaji nyambulishi ambavyo vilitamkwa na wazungumzaji wa KS, kurekodiwa kwenye kinasa sauti, na kuchakatwa kwa programu ya kompyuta ili kubainisha nyakaa za irabu zinazotokea kwenye matamshi hayo. Uchanganuzi wa data uliongozwa na kiunzi cha dhana ya urefu, urefushaji, na ufupishaji kama zinavyotumiwa katika fani ya fonolojia na fonetiki. Matokeo ya uchanganuzi huo yanaonesha kuwa viambishi {-z-, -ez-, -iz-} vinapoambatishwa kwenye mashina ya utenda ya vitenzi vya KS, urefu wa irabu za maumbo mapya ya vitenzi unaweza: (i) kutobadilika katika irabu yoyote; au (ii) kubadilika kwa kurefushwa kwa irabu fulani, hasa inayotokea kabla ya kiambishi tamati hicho, inayopakana nacho; au (iii) kubadilika kwa kufupishwa kwa irabu ndefu iliyopo kwenye umbo la utenda. Aidha, makala inaonesha kuwa vitenzi vya KS vinavyoishia na mlolongo wa irabu za chini, <-aa>, vinaweza kutofautiana sana na vitenzi vingine vya K.S. pindi vinapoambatishiwa viambishi-tamati vya utendeza, {-z-, -ez-, -iz-}, au viambishi vinginevyo.

Download

PDF