Abstract
Makala inajadili mikakati inayotumiwa na walimu na wanafunzi katika ufundishaji na ujifunzaji wa Kiswahili kama lugha ya pili katika shule teule za sekondari wilayani Musanze, nchini Rwanda. Licha ya jitihada za serikali za kukiendeleza Kiswahili tangu kutambuliwa kwake kama lugha rasmi mwaka 2017, ufundishaji wake bado unakabiliwa na changamoto mbalimbali, zikiwemo uhaba wa vifaa vya kielimu na walimu wenye weledi, mtazamo hasi kuhusu lugha ya Kiswahili, na kutokuwepo kwake katika mitihani ya taifa kwa ngazi ya chini ya sekondari. Utafiti uliongozwa na Nadharia ya Viwezeshi ya Gibson (1977). Mtafiti alitumia mbinu za ushuhudiaji na usaili, huku walengwa wakiwa walimu wa Kiswahili na wanafunzi kutoka Groupe Scolaire (G.S.) Muhoza I na Ecole de Sciences de Musanze (E.S.M.). Matokeo yalibaini mikakati mitano. Nayo ni: kuboresha makundi ya kujifunza ili kukabiliana na uhaba wa vitabu na kamusi, kuimarisha ushirikiano baina ya walimu kupitia mitandao ya kijamii, kutumia simu za mkononi kama teknolojia mbadala ya kufundishia, kuandaa mashindano na mijadala ya Kiswahili ili kujenga ujasiri wa kuongea, na kuhamasisha wanafunzi kuhusu umuhimu wa Kiswahili katika fursa za ajira na biashara. Matokeo yanathibitisha kuwa ingawa viwezeshi vya kimwili ni vichache, walimu wamefanikiwa kutumia viwezeshi vya kijamii na kisaikolojia kukabiliana na changamoto hizo.