Changamoto za Uandishi wa Miswada ya Filamu za Kiswahili Nchini Tanzania

Abstract

Makala hii inajadili changamoto za uandishi wa miswada ya filamu za Kiswahili nchini Tanzania. Msukumo wa utafiti wa makala ulichangizwa na maoni ya hadhira ambayo yalibainisha kutofuatiliwa kwa filamu za Kiswahili hutokana na udhaifu wa ujenzi na uwasilishwaji wa hadithi. Utafiti umetumia mikabala ya kihistoria, kiteknolojia, kibiashara na kimasoko kama kiunzi cha ukusanyaji, uchambuzi wa data na uwasilishaji wa matokeo. Mbinu za kitaamuli ndizo zimeendesha hatua zote za kitafiti. Makala inawasilisha changamoto mbalimbali zinazorudisha nyuma ubora wa miswada na filamu zinazotayarishwa. Nazo ni: ukosefu wa elimu na mafunzo ya uandishi wa miswada ya filamu kwa waandishi, ufinyu wa bajeti za kutayarishia filamu, kutofanyika kwa tafiti kabla ya uandishi wa miswada, pamoja na upungufu wa ubunifu wa uandishi wa miswada. Nyingine ni: mabadiliko ya mifumo ya mawasiliano ya kiteknolojia, ukosefu wa uhuru wa ubunifu, pamoja na udhaifu wa soko na hakimiliki. Ili kuboresha uandishi wa miswada ya filamu za Kiswahili nchini Tanzania, yafuatayo yanapendekezwa na makala hii: kutengenezwa kwa mitaala maalumu ya mafunzo kwa waandishi wa miswada ya filamu ili kuboresha uwezo wao, kutayarishwa kwa programu atamizi kwa waandishi wa miswada, idara zinazohusika na lugha na fasihi ya Kiswahili ziboreshe mitaala kwa kuihusisha fasihi na filamu, kuwapo kwa mashindano ya uandishi wa filamu za Kiswahili, pamoja na kurahisisha upatikanaji wa nyaraka za kitafiti ili kuboresha maandishi ya miswada kwa waandishi.

Download

PDF

Keywords

hadithi
,
filamu
,
mswada wa filamu