Abstract
Makala hii inafafanua dhana ya ukiushi wa kisintaksia katika tamthiliya ya Mashetani (1971) ya Ebrahim Hussein kama kisa mahsusi cha uchambuzi. Ukiushi hurejelea matumizi ya kimakusudi ya miundo inayokiuka kaida za kawaida za lugha ili kuibua athari za kimaana, kisaikolojia na kisanaa kwa hadhira. Ingawa dhana hii imejadiliwa kwa mapana katika taaluma ya elimumitindo, tafiti nyingi za Kiswahili zimejikita zaidi katika maudhui kuliko uchunguzi wa miundo ya lugha kama mbinu ya kisanii, hususan katika tamthiliya. Utafiti huu ulilenga kubainisha aina mbalimbali za ukiushi wa kisintaksia zilizotumiwa katika Mashetani na kueleza mchango wake katika kujenga dhamira za kazi husika. Tamthiliya iliteuliwa kwa kutumia usampulishaji lengwa kutokana na umahiri wake wa kimtindo na matumizi mapana ya lugha yenye ukiushi. Data zilikusanywa kwa njia ya usomaji makini wa matini na kuchanganuliwa kwa mkabala wa kitaamuli kwa kuongozwa na Nadharia ya Umtindo. Matokeo yanaonesha kuwa ukiushi wa kisintaksia ni mbinu muhimu ya kusisitiza maudhui na kuchochea tafakuri kuhusu masuala ya kijamii na kiitikadi. Makala hii inahitimisha kuwa uchambuzi wa miundo ya lugha ni muhimu katika kufichua maana za tamthiliya za Kiswahili na inapendekeza kuendelezwa kwa tafiti zaidi za kifani katika eneo hili.